Dawa gani nisitumie kama nina Kisukari?
Katika sayansi ya dawa kuna kitu kinaitwa muingiliano (drug interaction), hii inaweza kuwa muingiliano kati ya dawa na dawa, muingiliano kati ya dawa na ugonjwa, au muingiliano kati ya dawa na chakula.
Katika makala hii tutaangazia muingiliano wa dawa na ugonjwa wa kisukari pia muingiliano wa baadhi ya dawa na dawa za kisukari, kuna dawa ambazo zinaweza kusababisha sukari ya mwili kupanda, au dawa ambazo zinaweza kuzuia dawa zako za kisukari zisifanye kazi yake vizuri.
Kisukari ni nini?
Kisukari ni hali ambayo husababisha kiwango cha sukari katika damu kuwa juu isivyo kawaida. Kulingana na sababu zinazoweza kusababisha hali hii, kuna aina mbalimbali za kisukari:
Kisukari Aina ya 1 (Type 1 Diabetes)
Hii ni hali ambapo mwili hauwezi kuzalisha insulini kabisa. Hii ni kwa sababu seli za kongosho (pancreas) zinashambuliwa na mfumo wa kinga wa mwili na kuharibiwa. Hali hii inaweza kuwa ya kurithi na mara nyingi huanza utotoni au ujana, lakini inaweza kutokea kwa watu wa umri wowote.
Kisukari Aina ya 2 (Type 2 Diabetes)
Hii ni hali ambapo mwili unashindwa kutumia vizuri insulini (insulin resistance) au hauzalishi insulini ya kutosha. Aina hii ya kisukari mara nyingi huhusishwa na maisha ya mtindo duni, uzito wa kupindukia na historia ya familia.
Kisukari Cha Mimba (Gestational Diabetes)
Hii ni hali ambapo mjamzito anakuwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu, hii husababishwa na mwili wa mjamzito kushindwa kutumia insulini vizuri. Mara nyingi hali hii huanza kutokea kati ya wiki ya 24 na 28 ya ujauzito.
Dalili za Kisukari
- Kiu kali
- Kukojoa mara kwa mara
- Njaa isiyoisha
- Uchovu mwingi
- Kupungua uzito bila sababu
- Vidonda vinavyopona polepole
- Kuona ukungu
Dawa za kuepuka ikiwa una kisukari
STEROIDS
Steroids hasa zile zinazojulikana kama "corticosteroid" (prednisolone, dexamethasone na hydrocortisone), zinapotumiwa kwa muda mrefu au kwa dozi kubwa zina athiri jinsi mwili unavyo dhibiti kiwango cha sukari kwenye damu. Hii inaweza kuwa na athari kubwa kwa watu wenye kisukari au ambao wako kwenye hatari ya kupata ugonjwa huu.
Jinsi steroids zinavyoweza kuathiri viwango vya sukari
Huongeza kiwango cha sukari kwenye damu:
Pale kiwango cha sukari kwenye damu kinapokuwa juu, kongosho inatoa insulini, insulini itaenda kwenye ini na kutoa ishara ini liache kumwaga sukari kuingia kwenye mfumo wa damu, badala yake inaituma sukari kwenye seli moja kwa moja.
Dawa za steroids husababisha ini lisipokee taarifa ya insulini (aidha ni insulini iliyozalishwa na mwili au insulini inayotumika kama dawa na mgonjwa wa kisukari), na ini huendelea kumwaga sukari kwenye mfumo wa damu.
Matumizi ya steroids yanaweza yasihepukike kwa baadhi ya magonjwa, ndio maana ni muhimu kutoa taarifa kamili kwa daktari wako, ili aweze kufanya mabadiliko aidha kwenye dozi za steroids ama dawa zako za sukari.
Huongeza hamu ya kula
Steroids zinaweza kuongeza hamu yako ya chakula, hii inaweza kuchangia ongezeko la viwango vya sukari kwenye damu.
Hubadilisha usambazaji wa mafuta
Steroids hubadilisha jinsi mwili unavyo sambaza na kuhifadhi mafuta, zinaweza kusababisha mkusanyiko wa mafuta katika baadhi ya maeneo ya mwili kama vile uso, shingo na tumbo. Hali hii inajulikana kama "Cushingoid appearance"
BETA BLOCKERS
Dawa hizi hutumika kudhibiti shinikizo la damu (hypertension), mfano propranolol, atenolol na metoprol. Kwa wagonjwa wenye magonjwa yote mawili (Kisukari na Shinikizo la Damu) matumizi ya beta blockers yanaweza kuleta shida kwenye upande wa Kisukari.
Jinsi Beta Blockers zinavyoweza kuathiri matibabu ya kisukari
Zinaongeza hatari ya Sukari ya kiwango cha chini (Hypogylcemia)
Kwa mgonjwa wa Kisukari anayetumia dawa kama insulini au glimepiride kwa pamoja na beta blocker kama propranolol, anaweza asihisi mapema dalili za sukari ya chini hivyo kusababisha hypoglycemia kali.
Dalili kama vile mapigo ya moyo kwenda kasi, mitetemo, na wasiwasi hufichwa na matumizi ya beta blockers.
Pia beta blockers hudhoofisha uwezo wa ini kubadili "glycogen" kuwa "glucose", glycogen ni kama jenereta, inatoa huduma pale chanzo kikuu cha nishati kinapozidiwa, pale nishati ya haraka inapohitajika aidha uko mazoezini au kiwango cha sukari kimeshuka, glycogen huvunjwa na kubadilishwa kuwa sukari (glucose), hivyo kuigilia kati kwa mchakato huu kunaongeza hatari ya kupata hypoglycemia.
Hupunguza ufanisi wa insulini
Baadhi ya beta blockers mfano atenolol hupunguza ufanisi wa insulini, na hivyo kuongeza kiwango cha sukari kwenye damu na kufanya udhibiti wa kisukari kuwa mgumu zaidi.
Huongeza uzito
DAWA ZA AFYA YA AKILI
Dawa kama olanzapine, clazapine na risperidone zinaweza kuchochea kwa kiasi kikubwa athari za ugonjwa wa kisukari. Hivyo kuchukua tahadhari na kutoa taarifa kamili kuhusu historia ya mgonjwa ni hatua muhimu.
Jinsi dawa za afya ya akili zina athiri kisukari
Huongeza uzito
Olanzapine na Clozapine zinahusishwa na ongezeko kubwa la uzito aidha kwa kuongeza hamu ya chakula, ambapo mgonjwa atajikuta akila zaidi hasa vyakula vyenye sukari na mafuta mengi, au kupunguza shughuli za kimwili ambapo wagonjwa hukutana na hali za uchovu na usingizi, kupungua kwa shughuli za kimwili kunachochea ongezeko la uzito kwa sababu kiwango kidogo cha sukari kinatumika. Risperidone inaweza pia kuongeza uzito japo kwa kiasi kidogo, na kama tulivyoona awali ongezeko la uzito kupita kiasi kunaongeza upinzani wa insulini.
Huongeza viwango vya sukari mwilini
Olanzapine na Clozapine pia zinahusishwa na nafasi kubwa ya kuongeza kiwango cha sukari mwilini, vilevile zinaongeza nafasi ya mtu asiye na kisukari kupata ugonjwa huo. Risperidone inaweza kuongeza kiwango cha sukari ingawa kwa kiwango kidogo.
Huongeza kiwango cha lipidi
Olanzapine na Clozapine zinaweza kusababisha mabadiliko makubwa ya lipidi (cholesterol na triglyceride), na kuongeza hatari kwa wagonjwa wa kisukari kupata matatizo ya moyo na mishipa.
BAADHI YA DAWA ZA MAUMIVU
Dawa kama Ibuprofen, Aspirin na Naproxen. Hizi ni dawa za kupunguza maumivu na uvimbe (NSAIDs), kwa wagonjwa wa kisukari dawa hizi zinaweza kuathiri viwango vya sukari ama kuathiri jinsi dawa za kisukari.
Jinsi dawa za maumivu zinavyo athiri kisukari
Huathiri kazi ya figo
Ibuprofen, Naproxen na Aspirin zinaweza kudhoofisha kazi ya figo, jambo ambalo lina athiri jinsi dawa za kisukari zinavyoweza kutolewa mwilini na kusababisha madaliko yasiyo tabirika ya viwango vya sukari.
Ufuatiliaji wa karibu sana unahitajika kwa wagonjwa wa kisukari wanao tumia dawa hizi.
Hatari ya sukari ya kiwango cha chini (Hypoglycemia)
Dawa hizi zina hatari ya hypoglycemia (sukari ya kiwango cha chini) hasa pale zinapotumika na dawa za kisukari kama glipizide na insulini. Ufuatiliaji wa karibu wa viwango vya sukari na hali ya figo ni muhimu wakati wa kutumia dawa hizi.
DAWA ZA KUPUNGUZA CHOLESTEROL
"Statins" kundi la dawa zinazotumika kupunguza viwango vya cholesterol, matumizi yake kwa wagonjwa wa kisukari huja na tahadhari, kwani zinaweza kuathiri viwango vya sukari mwilini na kuongeza hatari ya kupata kisukari.
Jinsi statins zinavyo athiri viwango vya sukari
Hudhoofisha utoaji na kuongeza upinzani wa insulini
Tafiti zimeonesha kuwa baadhi ya statins hasa kwenye dozi kubwa zinahusishwa na ongezeko dogo la hatari ya kupata kisukari anina ya 2, mfano Atorvastatin, Rosulvastatin na Simvastatin.
Statins pia zinaweza kusababisha kuongezeka kidogo kwa viwango vya sukari ya kufunga (fasting blood glucose) na HbA1c (kipimo cha damu kinacho onesha wastani wa viwango vya sukari katika kipindi cha miezi miwili hadi mitatu) ambavyo ni vipimo vya udhibiti wa sukari kwa muda mrefu.
Hata hivyo mara nyingi faida za statins katika kupunguza hatari ya shambulio la moyo na kiharusi hupita hatari hizi, hasa kwa wagonjwa walioko kwenye hatari kubwa ya magonjwa ya moyo, lakini ufuatiliaji wa mara kwa mara wa viwango vya sukari ni muhimu kwa wagonjwa wa kisukari walioko kwenye dozi kubwa za statins.
Vitu vya kuzingatia kwa mgonjwa wa kisukari kabla ya kutumia dawa za magonjwa mengine
- Usitumie dawa yoyote bila ushari wa daktari
- Pima viwango vyako vya sukari mara kwa mara, angalau mara nne kwa siku au zaidi.
- Onana na daktari haraka ikiwa viwango vya sukari bado viko juu hata baada ya kutumia dawa zako za kisukari.
- Dhibiti ulaji wa vyakula vya wanga, na kufanya mazoezi kunasaidia kupunguza viwango vya sukari kwenye damu.
- Tembea na vitu vya dharura vya kusaidia kupandisha kiwango cha sukari mfano "glucose"
Comments
Post a Comment