ZIFAHAMU DAWA ZAKO
Poda za kuchanganya: Zitumike ndani ya siku 7 tu!
Dawa zilizotengenezwa kwa mfumo wa poda, mfano antibiotiki: amoxicillin, ampiclox, n.k. ukisha zichanganya na maji zinaweza kutumika ndani ya siku saba pekee. Baada ya siku saba uwezo wa dawa hizi kufanya kazi hupungua.
Baadhi ya dawa zina maelekezo ya kutunzwa kwenye jokofu (fridge), hivyo soma maelekezo kwenye boksi ama karatasi ya maelezo iliyo ndani ya boksi, ama muulize mtaalamu wa afya jinsi gani ya kuhifadhi dawa zako.
MUHIMU: Hakikisha unafunga vizuri chupa baada ya kila matumizi ili kuepuka kuingiza hewa na vijidudu.
Dawa za maji (syrup): Zitumike ndani ya siku 14 tu!
Dawa ambazo tayari ziko kwenye mfumo wa maji, mfano dawa za kikohozi za maji, baada ya kufunguliwa uwezo wake wa kufanya kazi unaanza kupungua baada ya siku kumi na nne.
Baada ya kufungua dawa hizi, hewa inayoingia inaweza kubadili maumbo ya kikemikali hivyo kadili dawa hizi zinavyo funguliwa uwezo wake unazidi kupungua.
MUHIMU: Hakikisha unafunga vizuri chupa baada ya kila matumizi ili kuepuka kuingiza hewa na vijidudu.
Dawa za macho na masikio: Zitumike ndani ya siku 30 tu!
Dawa za matone za macho na masikio zinaweza kutumika hadi siku 30 baada ya kufunguliwa, hii ni kwa sababu vihifadhio vya dawa hizi huanza kuisha nguvu baada ya siku hizi na kusababisha vijidudu kama bakteria kukua, hivyo inaweza kusababisha magonjwa mengine kama zikitumika.
MUHIMU: Hakikisha unafunga vizuri chupa baada ya kila matumizi ili kuepuka kuingiza hewa na vijidudu.
Dawa za kuhifadhi kwenye jokofu: Nyuzi joto 2-8
Baadhi ya dawa zinahitaji ubaridi ili kubaki kwenye viwango vinavyohitajika, dawa kama insulini za kisukari na baadhi ya dawa za macho na masikio, kiwango cha nyuzi joto kinatakiwa kusoma 2-8.
MUHIMU; Dawa hizi hazitakiwi kugandishwa, hivyo kutumia kipima joto maaulumu kinachoweza kupima joto ndani ya jokofu itasaidia.
Dawa za kupaka (TUBE)
Muda wa kutumia dawa za kupaka baada ya kufunguliwa hutegemea na dawa yenyewe, na maelekezo kutoka kwa mtengenezaji. Zifuatazo ni miongozo ya jumla kwa aina tofauti ya dawa za kupaka.
Dawa za ngozi za mafuta na krimu
- Matumizi baada ya kufunguliwa: Miezi 3 - 6
- Mapendekezo ya kuhifadhi: Hifadhi ikiwa imefungwa vizuri, mahali pakavu mbali na mwanga wa jua.
- Soma maelekezo kwenye kijikaratasi cha maelezo kwa taarifa zaidi.
Dawa za macho za mafuta
- Matumizi baada ya kufunguliwa: Wiki nne (siku 28)
- Mapendekezo ya uhifadhi: Soma maelekezo ya dawa husika, mara nyingi huwa sehemu kavu mbali na mwanga wa jua wa moja kwa moja, ila baadhi huitaji huitaji matunzo ya jokofu.
Jeli na mafuta za kinywa
- Matumizi baada ya kufunguliwa: Mara nyingi miezi 6
- Mapendekezo ya uhifadhi: Hifadhi ikiwa imefungwa vizuri, mahali pakavu mbali na mwanga wa jua.
NJIA SAHIHI ZA KUHIFADHI DAWA NYUMBANI
Dawa haziharibiki tu pale muda wake wa matumizi unapoisha (expire date), uhifadhi wa dawa hizi una husika kwa kiwango kikubwa katika kubakiza ubora wake.
Kumbuka kwamba dawa ni kemikali, na kemikali hubadilika mauombo yake kutengeneza kemikali nyingine zikikutana na vitu kama mwanga wa jua, joto na unyevunyevu.
- Hifadhi dawa mbali na mwanga wa jua
Mwanga wa jua ni moja ya kichocheo cha mabadiliko ya kikemikali, hivyo kuhifadhi dawa sehemu ambazo jua linaweza kupenya moja kwa moja, mfano dirishani, ni hatari kwa ubora wa dawa zako.
- HIfadhi dawa mbali na chanzo cha moto
Kama ilivyo kwa mwanga wa jua, joto pia ni kichocheo cha mabadiliko ya kikemikali, hivyo kuhifadhi dawa sehemu zilizoko karibu na chanzo cha moto kama jikoni, ni hatari kwa ubora wa dawa.
- Hifadhi kwenye kifungashio asili cha dawa
Baadhi ya dawa zinaweza kuathiriwa na aina ya kifungashio (container) ama vifungashio havikidhi mahitaji ya dawa, hivyo kusababisha dawa kuharibika kabla ya muda wake na zinaweza kuleta madhara kama zikitumika.
Mfano, dawa zinazohifadhiwa kwenye "blister" (amoxicillin, n.k) zikiwekwa nje ya blister zinaweza kunyonya unyevu kutoka hewani na kuharibu dawa, ama dawa zinazohifadhiwa kwenye makopo kama virutubisho (supplements) zikiwekwa kwenye bahasha za kawaida zinaharibika mapema kutokana na kuwa wazi kwenye uwepo wa hewa na mwanga wa jua.
- Usihifadhi dawa bafuni
Bafuni kuna unyevunyevu na joto, vyote hivi ni adui wa dawa. Japo imeonekana ni kawaida kuhifadhi dawa zetu eneo hili, kwa ubora wa dawa na kwa afya zetu eneo hili si salama. - Soma maelekezo katika vifungashio vya dawa
Hakikisha unasoma maelekezo ya jinsi ya kuhifadhi dawa zako katika vifungashio husika, kulingana na aina ya dawa ama watengenezaji kunaweza kua na mahitaji maalumu ya kutunza dawa zako, hivyo soma maelekezo vizuri.
Hitimisho:
Ni muhimu kuelewa dawa ni kemikali, na zinaweza kubadilika zikiathiriwa na vichocheo kama joto, mwaga wa jua, unyevu na hewa. Hivyo kuhifadhi dawa zako kwa njia sahihi ni hatua mojawapo ya kulinda afya yako.
Hakikisha unafuata maelekezo ya ya mtengenezaji kwa kusoma karatasi ya maelezo iliyomo kwenye kifungashio, ama fuata maelekezo ya mtaalamu wa dawa.
Comments
Post a Comment