p2 ni nini?
"Morning pills" ama "p2" kama zinavyofahamika na watu wengi mtaani, ni dawa za dharura zinazotumika kuzuia mimba. p2 zina homoni inayoitwa "levenogesterol" ambayo hufanya kazi ya kuzuia mimba kwa njia kuu tatu:
- Huzuia yai kutolewa (Ovulation)
- Huzuia mbegu ya kiume kukutana na yai (Fertilization)
- Huzuia yai lililotungwa kujishikiza kwenye mji wa uzazi (Implantation)
Dawa hizi ni kwa ajili ya dharura tu, na hufanya kazi ndani ya masaa 72 baada ya kufanya tendo ka ndoa bila kinga, ufanisi wake unaweza kufika hadi asilimia 95 ikiwa zitatumika mapema.
Mara ngapi nitumie p2?
Ni salama kutumia p2 mara moja katika mzunguko mmoja wa hedhi, matumizi ya mara nyingi ndani ya mzunguko mmoja wa hedhi yanaweza kusababisha madhara makubwa zaidi ya homoni na mzunguko wa hedhi.
Matumizi ya mara kwa mara yanaweza kusababisha mzunguko wa hedhi usio tabirika, kutokuwepo kwa hedhi kwa muda mrefu, au kutokwa na damu isiyo kawaida (spotting).
p2 zinabeba dozi kubwa ya homoni (levenogesterol) ambayo inaweza kuvuruga mzunguko wa kawaida wa homoni mwilini. Hii inaweza kusababisha kubadilika kwa hedhi, maumivu ya kichwa na hisia za kuchoka au kukosa nguvu.
p2 inaweza kusababisha utasa?
Hapana! Matumizi ya p2 yanaweza kusababisha madiliko ya mzunguko wa hedhi au kutokuwepo kwa hedhi kwa muda, lakini hayaathiri uzazi wa muda mrefu. Uwezo wa kupata mimba utarejea mara tu baada ya mzunguko wa hedhi kurudi.
p2 inaweza kusababisha saratani?
Hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoonesha dawa hizi zina uhusiano na saratani ya ovari, matiti, shingo ya kizazi au mfuko wa kizazi.
Homoni iliyomo kwenye dawa za p2 ni sawa na iliyomo kwenye dawa za uzazi wa mpango (COC), ingawa matumizi ya muda mrefu (miaka mitano au zaidi) ya COC yanahusishwa na kuongezeka hatari ya kupata saratani ya matiti au saratani ya shingo ya kizazi, kwa p2 kwasababu matumizi yake ni ya muda mfupi, hayajatajwa kuongeza hatari ya saratani ya aina yoyote.
Comments
Post a Comment