Skip to main content

Nyama Nyekundu na Hatari Zake!

 

Hatari za Afya Zinazohusiana na Ulaji wa Nyama Nyekundu

Nyama nyekundu, kama vile nyama ya ng’ombe, mbuzi, na kondoo, ni chanzo kizuri cha protini, madini ya chuma, na zinki. Hata hivyo, ulaji mwingi wa nyama nyekundu umehusishwa na hatari mbalimbali za kiafya. 

Makala hii inakufahamisha zaidi kuhusu hatari hizi na jinsi unavyoweza kuboresha lishe yako kwa njia salama.


1. Magonjwa ya Moyo

Nyama nyekundu, hasa iliyo na mafuta mengi, inaweza kuongeza hatari ya magonjwa ya moyo.

2. Kansa ya Utumbo Mkubwa (Colon Cancer)

Utafiti umeonyesha kuwa ulaji wa nyama nyekundu, hasa iliyosindikwa kama sausage na bacon, unaongeza hatari ya kansa ya utumbo.

  • Nyama zilizochakatwa: Matumizi ya mara kwa mara ya "sausage" na "bacon" yanahusishwa na saratani ya utumbo mpana (colorectal cancer)
  • Mbinu za kupika: Kupika nyama kwa joto la juu (kama kukaanga au kuchoma) huzalisha kemikali hatari kama (heterocyclic amines) HCAs na (polycyclic aromatic hydrocarbons) PAHs, ambayo inaweza kuongeza hatari ya kupata saratani. 

3. Hatari ya Kisukari

Tafiti zinaonesha ulaji wa nyama nyekundu, hasa zilizosindikwa huongeza hatari ya mwili kuwa sugu kwa insulini, hali inayoweza kupelekea kisukari cha aina ya pili (Type 2 Diabetes)

4. Madhara kwenye Figo na Ini

Protini nyingi kutoka kwenye nyama nyekundu inaweza kuongeza mzigo kwa figo na ini.

  • Kazi ya ziada: Figo zinapofanya kazi zaidi kuchuja protini, zinaweza kuchoka, hasa kwa wale walio na matatizo ya figo tayari.
  • Fatty acid: Nyama nyekundu ni chanzo kikubwa cha "saturated na monosaturated fatty acids" mafuta haya yanaweza kujikusanya kwenye ini na kusababisha ugonjwa wa "NonAlcoholic Fatty Liver Disease". 

5. Hatari ya Afya ya Mifupa

  • Ongezeko la uric acid: Ulaji wa nyama nyekundu, hasa maini na figo unaweza kupelekea ongezeko la uric acid mwilini na kusababisha ugonjwa wa gout, aina ya arthritis inayosababisha maumivu makali na uvimbe kwenye viungo. 
  • Upungufu wa uzito wa mifupa: Ulaji wa nyama nyekundu bila kuchanganya na vyakula vyenye hali ya alkali kama matunda na mboga mboga, unaweza kufanya mwili kuwa na hali ya asidi kupita kiasi (acidic body condition). Hali hii husababisha:
    • Mwili kutoa calcium kwenye mifupa ili kusaidia kupunguza asidi hiyo, hatua ambayo huathiri afya na nguvu ya mifupa. 
    • Hali ya upungufu wa calcium huongeza hatari ya kupungua kwa uzito wa mifupa (osteoporosis)  na hivyo kusababisha mifupa kuwa dhaifu na rahisi kuvunjika. 

Je nyama nyekundu zote zina madhara sawa?

Nyama nyekundu zilizochakatwa

  • Hizi ni hatari zaidi kutokana na vihifadhio vinavyoongezwa na kiwango kikubwa cha sodium. 
  • Mfano: bacon, sausage, na nyama za kwenye makopo.
Nyama zisizochakatwa (Asilia)
  • Zina madhara kama zikitumika kwa kiwango kikubwa, ila si hatari sana ukilinganisha na nyama iliyochakatwa. 
  • Mfano: nyama za ng'ombe, mbuzi na kondoo
Nyama iliyotokana kwa wanyama waliofugwa kwa nyasi (grass-fed)
  • Huwa na mafuta kidogo (saturated fat) kulinganisha na nyama iliyotoka kwa wanyama waliofugwa kwa nafaka. 
  • Zina virutubisho vya omega-3 fatty acids, ambazo husaidia kupunguza hatari ya uvimbe na magonjwa ya moyo. 
Nyama iliyotokana na wanyama waliofugwa kwa nafaka (grain-fed)
  • Zina kiwango cha juu cha omega-6 fatty acids, ambazo zikitumika kupita kiasi zinaweza kuchochea uvimbe mwilini. 
  • Zina kiwango kikubwa cha mafuta (saturated fat), ambazo huongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo zikitumika kupita kiasi. 

Vidokezo vya kupunguza hatari!

  • Punguza kiwango: usizidishe vipande 6 (ukubwa wa kipande cha  mama lishe) kwa wiki, sawa na kula nyama mara tatu kwa wiki. 
  • Badilisha njia za kupika: Pika kwa kuchemsha au kuoka badala ya kukaanga au kuchoma. 
  • Chagua sehemu zenye mafuta kidogo: kama vile nyama ya kwenye miguu, au nyama laini (sirloin)
  • Jumuisha vyakula vya mimea: Ongeza maharage, njegere, na mbegu mbegu kwenye lishe yako kama chanzo mbadala cha protini. 

Anza kupunguza ulaji wa nyama nyekundu, badilisha na vyakula kama vile samaki, kuku, maharage au mboga za majani. 
Je tayari umeanza kupunguza ulaji wa nyama nyekundu? Tuambie changamoto zako na mbinu unazotumia kwenye safari yako ya kuboresha afya!  

Comments